8 Oktoba 2025 - 09:55
Jeshi la Majini la Israel lavamia Msafara wa Uhuru uliokuwa ukielekea Gaza

Msafara wa Kimataifa wa Ustahimilivu (al-Sumud) umetangaza kuwa Jeshi la Majini la utawala wa Kizayuni limeushambulia Msafara wa Uhuru uliokuwa ukielekea Gaza kwa lengo la kuvunja mzingiro unaoendelea dhidi ya eneo hilo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Msafara wa Kimataifa wa Ustahimilivu ulitangaza kupitia ukurasa wake wa X mapema Jumatano kwamba Jeshi la Majini la Israel limeushambulia Msafara wa Uhuru uliokuwa ukielekea Gaza.

Kamati ya Kimataifa ya Kuvunja Mzingiro wa Gaza imesema kuwa jeshi la uvamizi limeushambulia msafara huo katika maji ya kimataifa, umbali wa takribani maili 120 (sawa na kilomita 222) kutoka Ukanda wa Gaza.

Kamera za ufuatiliaji za Msafara wa Uhuru zimeonyesha picha za askari wa Israel wakipanda kwenye meli kadhaa na kuwakamata washiriki wa msafara huo.

Shirika la habari la Reuters likinukuu uongozi wa Msafara wa Uhuru, liliripoti kuwa jeshi la Israel limekuwa likizua usumbufu wa mawimbi ya mawasiliano na limepanda angalau kwenye meli mbili.

Wakati huo huo, Reuters ilinukuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel ikidai kwamba meli na abiria wa Msafara wa Uhuru “wako salama na wanapelekwa katika bandari ya Israel”.

Wizara hiyo imedai kuwa abiria wa msafara huo watafukuzwa mara moja, ikieleza kuwa juhudi za Msafara wa Uhuru ni “jaribio jingine lisilo na maana la kuvunja mzingiro wa baharini na kuingia kwenye eneo la vita bila mafanikio yoyote.”

Msafara huo wenye meli 11 ulianza safari yake miezi 25 iliyopita kutoka Italia.

Kabla ya tukio hili, Kituo cha Televisheni cha Channel 13 cha Israel kiliripoti kuwa jeshi la nchi hiyo lilikuwa likiandaa mpango wa kuzikamata meli nyingine zilizotoka Italia na zinatarajiwa kufika Gaza usiku wa leo.

Televisheni hiyo, ikinukuu vyanzo vya usalama, ilisema kuwa kukabiliana na msafara huu mpya kunaweza kuwa jambo gumu zaidi.

Meli za muungano wa Msafara wa Uhuru, baada ya kuondoka kisiwa cha Sicily, Italia miezi 25 iliyopita, zilielekea moja kwa moja Gaza, licha ya upinzani uliopo. Waandaaji wa kampeni hiyo walisisitiza kuwa wataendelea na juhudi zao kufika Gaza.

Meli al-Dhamir, mojawapo ya meli za msafara huo, ilikuwa imebeba waandishi wa habari na wahudumu wa afya kutoka nchi 25 tofauti. Wasaidizi hao na wawakilishi wa vyombo vya habari walikuwa wakielekea kuungana na wenzao katika Msafara wa Uhuru kwa lengo la kuvunja mzingiro wa Gaza unaofanywa na Israel.

Meli al-Dhamir iliwahi kushambuliwa na wanajeshi wa Israel katika pwani ya Malta mwezi Mei uliopita.

Jumatano iliyopita jioni, Jeshi la Majini la Israel lilishambulia Msafara wa Kimataifa wa Ustahimilivu uliokuwa ukielekea Gaza, likiwakamata mamia ya wanaharakati waliokuwa katika meli 42 na baadaye kuwaachia wengi wao.

Wanaharakati wa kimataifa waliokamatwa walihamishiwa gerezani Ketziot kusini mwa Israel kabla ya kuanza mchakato wa kuwafukuza nchini humo.

Msafara wa Uhuru, pamoja na ule wa Kimataifa wa Ustahimilivu uliyoanza safari mwishoni mwa mwezi Agosti, ni juhudi za hivi karibuni za wanaharakati kuupinga mzingiro wa baharini dhidi ya Ukanda wa Gaza unaofanywa na Israel — mzingiro ambao umepelekea mauaji ya zaidi ya watu 67,000, majeruhi kwa maelfu, uharibifu mkubwa wa miundombinu na janga la kibinadamu lisilokuwa na mfano katika historia ya hivi karibuni.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha